Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WIZARA YAANZA TATHMINI YA MIAKA MITANO YA UTENDAJI KAZI NGOs

Imewekwa: 10 Dec, 2025
WIZARA YAANZA TATHMINI YA MIAKA MITANO YA UTENDAJI KAZI NGOs

Na WMJJWM - Morogoro

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) imeanza zoezi la kufanya tathmini ya utendajii kazi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kwa kipindi cha miaka mitano 2020/2021 - 2024/2025.

Lengo la zoezi hili ni kutathmini mchango wa NGOs katika utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali, uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazosimamia NGOs, utekelezaji wa Mwongozo wa Uratibu wa NGOs Tanzania Bara na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs, pamoja na utekelezaji wa majukumu ya Bodi ya Uratibu wa NGOs na Baraza la Taifa la NGOs.

Timu ya Wataalam kutoka Wizarani iliyoongozwa na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Mkuu wa Idara ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Charles Komba imeanza kazi hiyo Disemba 1 - 3, 2025 mkoani Morogoro kwa kufanya uchambuzi wa nyaraka mbalimbali ambazo zimetoa picha halisi ya mafanikio, changamoto, fursa na matarajio ya Mashirika hayo katika kuongeza ufanisi na utambuzi wa mchango wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Komba amesema wanafanya tathmini hiyo ili kujua kwa kina mchango wa Mashirika hayo katika Maendeleo ya Taifa, ambapo pamoja na zoezi hilo wamepata nafasi ya kusikia ushuhuda kutoka kwa wanufaika wa huduma mbalimbali zinazotolewa na Mashirika hayo hususani katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

“Tumefanikiwa kutembelea miradi na kuzungumza na wananchi walionufaika na huduma zinazotolewa na mashirika manne: Kinara For Youth Evolution inayotoa mafunzo ya ushonaji kwa wasichana, taulo za kike kwa wanafunzi na mtandao wa elimu ya kujikinga na vihatarishi vya mimba za utotoni na vijana kujiepusha na makundi hatarishi;