WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA MWONGOZO WA UENDESHAJI WA BARAZA LA NaCoNGO TOLEO LA PILI
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Toleo la Pili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo tarehe 25, 2026 jijini Dodoma, Dkt. Gwajima amesema mwongozo huo umeandaliwa ili kuainisha taratibu, majukumu, wajibu na mfumo wa uendeshaji wa Baraza kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwazi na uwajibikaji kwani mwongozo huo umeboreshwa ili kuendana na mabadiliko ya kisheria na mazingira ya sasa ya utendaji, na utasaidia kuimarisha uongozi na ufanisi wa Baraza kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi Taifa.
Aidha, Dkt. Gwajima amewataka viongozi na wajumbe wa NaCoNGO kuhakikisha mwongozo huo hauishii kuwa nyaraka za ofisini, bali unawafikia wanachama wote kupitia elimu na mafunzo ili ueleweke na kutekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amewataka viongozi wa NaCoNGO kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwazi huku wakiepuka ukiritimba na vikwazo visivyo vya lazima vinavyoweza kudhoofisha utendaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali huku akisema uongozi unaozingatia ushirikiano utaongeza ufanisi wa sekta hiyo katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na kuimarisha mazingira ya utendaji wa mashirika hayo kupitia maboresho ya mifumo ya usimamizi.ñ hivyo Baraza litasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mwongozo huo kwa kuhakikisha viongozi na wanachama wanapatiwa elimu ya kutosha kuhusu maudhui yake ili uwe chachu ya uwajibikaji, uwazi na ushirikiano wenye tija katika kuleta maendeleo ya Taifa.