WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA KITINI CHA MAFUNZO YA UANDAAJI WA BAJETI YENYE MRENGO WA KIJINSIA (GRB)
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua kitini cha mafunzo ya uandaaji wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia (Gender Responsive Budgeting) akisisitiza umuhimu wa mipango na bajeti za taifa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchochea maendeleo jumuishi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa wabunge jijini Dodoma, Dkt. Gwajima amesema bado kuna pengo la kijinsia katika upangaji na utekelezaji wa bajeti. Amebainisha kuwa wanawake wengi hususan vijijini, hukosa fursa muhimu kama mikopo, pembejeo na masoko licha ya mchango wao mkubwa katika sekta ya kilimo.
Ameeleza kuwa matumizi ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia yameleta mafanikio katika nchi mbalimbali zikiwemo Rwanda na Uganda, na kuwataka wabunge kutumia nafasi zao kuchambua na kufuatilia bajeti kwa mtazamo wa kijinsia ili kupunguza na hatimaye kuondoa ukosefu wa usawa.
Aidha, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa kitini hicho kitakuwa nyenzo muhimu kwa wadau wa bajeti nchini, kikilenga kuongeza ufanisi katika upangaji na utekelezaji wa sera na mipango inayogusa wananchi wote bila ubaguzi wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mwezeshaji na Mkufunzi wa masuala ya jinsia, Dkt. Suma Kaare, amesema ni muhimu kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Ametaja baadhi ya vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na mila na desturi za mfumo dume, ushiriki mdogo wa wanaume katika kukuza usawa wa kijinsia, uwepo wa sheria na sera zisizotekelezwa kikamilifu, pamoja na uhaba wa bajeti kwa programu za usawa wa kijinsia.
Naye Mkuu wa Idara ya Sera, Mkakati na Ubora kutoka Shirika la Plan International, Christina Ruhinda, amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha usawa wa kijinsia katika mipango na matumizi ya rasilimali za umma. Aidha, ameahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na Bunge katika kujenga Tanzania yenye maendeleo jumuishi, yenye haki na usawa wa kijinsia.
MWISHO