WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA KITAIFA YA KUHAMASISHA MAADILI NA MALEZI CHANYA KWA WATOTO
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Handeni, Tanga
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi Kampeni ya Kitaifa ya Maadili na Malezi Chanya kwa Watoto kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, kampeni itakayotekelezwa nchi nzima hadi Juni 30, 2026.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mei 24, 2026, Dkt. Gwajima amesema kampeni hiyo inayobebwa na kaulimbiu isemayo “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara” (Tuanzie nyumbani) inalenga kuhamasisha wazazi, walezi na jamii kuhusu umuhimu wa malezi chanya katika maendeleo na ustawi wa mtoto, familia na Taifa, pamoja na kujenga kizazi chenye maadili mema na uwajibikaji kuanzia ngazi ya familia.
Aidha, Dkt. Gwajima amekemea matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayochangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana, akieleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakijiingiza katika tabia ovu kupitia majukwaa ya kidijitali kutokana na kukosa mwongozo na usimamizi wa wazazi au walezi. Pia amewataka watoto kujilinda dhidi ya ukatili wa mtandaoni kwa kutokutuma picha za utupu au taarifa binafsi kwa watu wasiowafahamu, wakiwemo wanaojiita wapenzi wao.
Vilevile, Dkt. Gwajima amewataka viongozi wa Serikali katika ngazi zote kuhakikisha ajenda za malezi na makuzi bora ya watoto, ulinzi, usalama na maadili zinajadiliwa katika vikao vya mabaraza ya kata na mamlaka nyingine za maamuzi, sambamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati. Amesisitiza kuwa malezi ya watoto si ajenda ya ziada bali ni msingi wa kulinda kizazi kijacho na ustawi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amesema Wilaya hiyo imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na kwamba yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na viongozi wa kata, vijiji pamoja na wadau wa maendeleo. Amesema wataendelea kuimarisha ajenda za malezi, maadili, ulinzi na usalama wa watoto katika vikao vya Serikali za Mitaa sambamba na kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao na mapambano dhidi ya ukatili kwa watoto.
MWISHO