Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA ATOA WITO KWA WAZAZI NA WALEZI KUSIMAMIA MAADILI MEMA KWA WATOTO

Imewekwa: 25 May, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA ATOA WITO KWA WAZAZI NA WALEZI KUSIMAMIA MAADILI MEMA KWA WATOTO

Na Saidi Saidi, WMJJWM, Korogwe - Tanga

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi ya maadili mema, upendo na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili, akisisitiza kuwa malezi bora ndiyo msingi wa kujenga Taifa imara.

Dkt. Gwajima amesema hayo Mei 23, 2026 akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Korogwe mkoani Tanga ya kuhamasisha maadili na malezi chanya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yatakayofanyika Mei 30, 2026.

Katika hotuba yake, Dkt. Gwajima amesema jamii kuzingatia malezi chanya na maadili mema ni jambo muhimu kwani ni utekelezaji wa nguzo ya pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohusu Uwezo wa Watu na Maendeleo ya Jamii. Amesema nguzo hiyo inalenga kujenga rasilimali watu yenye ujuzi, maisha yenye staha, usawa na utu kupitia malezi bora ya watoto, elimu na mafunzo bora, huduma za afya, pamoja na mifumo jumuishi ya hifadhi ya jamii.

Aidha, ameeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayochangia mmomonyoko wa maadili, mimba za utotoni na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima ametangaza uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Maadili na Malezi Chanya kwa Watoto itakayozinduliwa Mei 24, 2026 wilayani Handeni chini ya kaulimbiu isemayo “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara.” Amesema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa malezi bora kuanzia utotoni ili kujenga kizazi chenye maadili mema, uzalendo na uwajibikaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Korogwe Mhe. Salum Nyamwese, amesema Wilaya hiyo imejipanga kushiriki kikamilifu Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu malezi bora, maadili mema na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake.

 

slot gacor