WAZIRI DKT. GWAJIMA APONGEZA SHIRIKA LA BRAC MAENDELEO KUIMARISHA MIRADI YA MALEZI NA MAKUZI BORA YA WATOTO NCHINI.
AWATAKA VIONGOZI KUBEBA AJENDA HIYO NA KUSIMAMIA UANZISHWAJI WA VITUO VYA MALEZI NA MAKUZI
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Iringa
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amelipongeza Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha malezi na makuzi bora ya watoto, akisema uwekezaji huo ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili, fikra chanya na uwajibikaji kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo Julai 11, 2026 mkoani Iringa, wakati wa kikao cha majumuisho kilichowakutanisha viongozi wa Mkoa wa Iringa na Shirika la BRAC Maendeleo Tanzania kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na shirika hilo. Kikao hicho kimefanyika mara baada ya ziara yake ya kutembelea na kujionea utekelezaji wa miradi hiyo, ambapo amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika vituo vya malezi na makuzi pamoja na mabadiliko chanya yanayoonekana kwa watoto, huku akilipongeza shirika hilo kwa kufanikisha kuanzishwa kwa vituo 162 tangu kuanza kwa programu hiyo mwaka 2023.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Gwajima amewataka viongozi kubeba ajenda ya malezi na makuzi bora ya watoto na kusimamia uanzishwaji wa vituo zaidi katika maeneo yao, akihimiza angalau kila mtaa kuwa na kituo cha kijamii cha malezi na makuzi ya watoto. Amesisitiza kuwa maendeleo ya kiuchumi yanapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya malezi na makuzi, akieleza kuwa Taifa haliwezi kufikia maendeleo endelevu bila kujenga kizazi chenye maadili mema, fikra chanya, uzalendo na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, mhe. Benjamin Sitta, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James, amesema Serikali ya Mkoa imepokea maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Gwajima na itaendelea kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali na wadau, ili kuimarisha huduma za malezi na makuzi bora ya watoto mkoani humo.