WAZIRI DKT. GWAJIMA APONGEZA MCHANGO WA SHIRIKA LA WORLD VISION KATIKA MAENDELEO NA USTAWI WA JAMII
Na WMJJWM – Tanga
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameipongeza World Vision Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi na ustwi wa jamii, akisisitiza kuwa miradi inayotekelezwa inalenga moja kwa moja ustawi wa watoto, wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum.
Dkt. Gwajima amesema hayo Februari 23, 2026 katika ziara yake ya kutembelea miradi inayotekelezwa na shirika hilo mkoani Tanga katika Kijiji cha Mnyuzi, wilayani Korogwe.
Dkt. Gwajima ameridhishwa na maboresho ya huduma za afya kupitia ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya Zahanati ya Mnyuzi. Amesema hatua hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma za afya kutoka wananchi 421 mwaka 2020 hadi 1,790 mwaka 2023, huku kwa sasa zahanati hiyo ikihudumia zaidi ya wananchi 7,600 kutoka vijiji sita vinavyoizunguka.
Kwa upande wa elimu, Waziri Gwajima amesema usaidizi wa World Vision Tanzania katika ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vyoo, vituo vya kunawia mikono pamoja na upatikanaji wa madawati umeleta mapinduzi makubwa katika mazingira ya kujifunzia. Ameeleza kuwa jitihada hizo zimepunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kuchangia ongezeko la ufaulu wa Darasa la Saba hadi zaidi ya asilimia 95 kwa miaka mitatu mfululizo.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. William Simon Mwakilema, amesema Serikali ya Mkoa wa Tanga itaendelea kushirikiana kwa karibu na World Vision Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Ameongeza kuwa Mkoa huo utaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kupinga vitendo vya ukatili na kukomesha tabia zote za uvunjifu wa maadili katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa World Vision Tanzania, James Anditi, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaoupata katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuibua na kutekeleza miradi endelevu itakayochangia kuboresha afya, elimu na uchumi wa kaya, hususan kwa watoto na makundi yaliyo hatarini.