Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AMPOKEA RAIS MSTAAFU WA LIBERIA  MHE. ELLEN JOHNSON SIRLEAF  KWA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Imewekwa: 20 Apr, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA AMPOKEA RAIS MSTAAFU WA LIBERIA  MHE. ELLEN JOHNSON SIRLEAF  KWA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

Na Saidi Saidi WMJJWM - Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, akiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa James Kinyasi Millya, wamempokea Rais Mstaafu wa Liberia, Mheshimiwa Ellen Johnson Sirleaf, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kuwasili nchini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam leo Aprili 19, 2026


Rais huyo wa zamani wa Liberia, ambaye pia ni mlezi wa Mtandao wa Wanawake Viongozi Barani Afrika (African Women Leaders Network - AWLN), amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Aprili 19 hadi 22, 2026.

Akiwa nchini, Mheshimiwa Sirleaf anatarajiwa kushiriki mkutano wa Kamati ya Uongozi ya AWLN pamoja na kukutana na viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya siasa na wanawake kutoka sekta mbalimbali. Ziara hiyo inalenga kukuza usawa wa kijinsia, utawala bora, kuwawezesha wanawake na kuhimiza maendeleo jumuishi.

Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika (AWLN) ulianzishwa kwa lengo la kukuza sauti na ushawishi wa wanawake katika nafasi za uongozi, na umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuunda sera zinazowezesha wanawake kisiasa, kiuchumi na kijamii.