Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AITAKA NACONGO KUWAJIBIKA NA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SERIKALI.

Imewekwa: 24 Apr, 2026
WAZIRI DKT. GWAJIMA AITAKA NACONGO KUWAJIBIKA NA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SERIKALI.

Na Oscar Tarimo WMJJWM - DODOMA.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka viongozi wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katika majukumu yao kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliofanyika Aprili 22, 2026 jijini Dodoma, Dkt. Gwajima amesema, mashirika hayo yanapaswa kuwekewa mazingira wezeshi ili kuinua zaidi ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa ushirikiano zaidi na wadau wote wa kisekta ngazi zote za mamlaka za serikali.

"tutaendelea kuyawekea mazingira Bora zaidi Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaendelee kutimiza wajibu wao kwa ufanisi zaidi ili kuchochea Kasi ya utekelezaji kuelekea Dira ya Maendeleo 2050," alisema Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima ameipongeza Kamati ya kisekta ya kushughulikia changamoto za NACONGO kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto 15 kati ya 19 huku akiahidi kuhakikisha kuwa, hata 4 zilizobakia zitaendelea kufanyiwa kazi kadri inavyostahili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Ndugu Jasper Makala, amemshukuru Waziri Gwajima kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo. Aidha, ameeleza baadhi ya changamoto zinazowakabili, ikiwemo upatikanaji mdogo wa rasilimali fedha, uelewa mdogo wa baadhi ya wadau kuhusu majukumu ya mashirika yasiyo ya kiserikali, pamoja na changamoto za uratibu katika baadhi ya maeneo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waheshimiwa Wabunge kwa tiketi ya Mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwemo Mhe. Ryadhi Kisuo, Naibu Waziri wa Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Uhusiano, Mhe. Asha Baraka pamoja na Mhe. Margareth Ezekiel.