WAZEE WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUBORESHA HUDUMA KWA USTAWI WAO.

na WMJJWM-Dodoma
Wazee wameshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira mazuri katika utoaji wa huduma za Afya kwa wazee na masuala mengine ya Ustawi wao.
Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha Wazee Tanzania (CCWWT) Tadey Mchena alipokutana na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu Juni 04, 2025 jijini Dodoma.
Mchena amesema katika kipindi cha miaka minne (4) ya Uongozi wa Rais Samia huduma zinazotolewa kwa Wazee zimeboreshwa hasa utoaji wa vitambulisho vya Bima kwa Wazee ili kupata huduma bora.
"Tunamshukuru sana Mhe Rais wa Jamhuri wa Muungano Kwa kujali na kuthamini Wazee mara kadhaa wa kadha amewatuma wasaidizi tuseme tu ametubeba Wazee katika masuala yanayotuhusu hasa katika huduma za Afya katika maneno tulipo". amesisitiza Mchena.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. John Jingu amesema Serikali kupitia Wizara inathamini wazee na itaendelea kuwapatia huduma stahiki katika maneno mbalimbali kwa sababu ni hazina ya Taifa.
"Niwashukuru wazee kwa kuja kuzungumza na Wizara yenu na niwaahidi mapendekezo na maoni yamepokelewa na yatafanyiwa kazi ili kustawisha maisha ya wazee nchini kote" amesisitiza Dkt. Jingu
Aidha Dkt Jingu amewapatia miongozo na vitini mbalimbali vinavyohusu ustawi wa wazee, haki zao pamoja na kuwaomba kusoma ili waweze kuwaelimisha wazee ndani ya chama na nje ya chama chao.