WAZEE WAHESHIMIWE, KUENZIWA - MAHUNDI
Na Jackline Minja, WMJJWM
Dar Es Salaam
Serikali imesema itaendelea kuimarisha huduma za afya, hifadhi ya jamii na ustawi wa wazee nchini ili kuwawezesha kuishi maisha yenye heshima, usalama na furaha, sambamba na kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi wa taifa.
Akizungumza na wanachama wa Klabu ya Wazee Msasani mkoani Dar Es Salaam, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Wazee ni miongoni mwa makundi maalum ambayo Serikali imeendelea kuyawekea mkazo kwa kuweka Sera, Mipango na Mikakati madhubuti inayolenga kuhakikisha Wazee wanapata haki zao kikamilifu ikiwa dhamira hii inaenda sambamba na juhudi za kuboresha ustawi wao kijamii, kiafya, kiuchumi na kiakili, ili kuhakikisha wanazeeka kwa heshima, utu na maisha yenye thamani.
“Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini mchango wa wazee katika maendeleo ya nchi yetu, ndiyo maana inaendelea kuhakikisha wanapata huduma muhimu ikiwemo matibabu, hifadhi ya jamii na mazingira rafiki ya kuishi, Wazee ni tunu ya taifa letu kwa sababu uzoefu na hekima yao vina mchango mkubwa katika kujenga na kuimarisha jamii,” amesema Mahundi.
Amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wazee wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuwaheshimu na kuwajali wazee kama sehemu ya kutambua mchango wao.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wazee wenzake Atanasi Michael ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na kuwathamini, huku akisema hatua hiyo imeongeza ari na kuwapa matumaini ya kuendelea kuishi kwa furaha na kushiriki katika maendeleo ya jamii.
“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kututhamini na kutupa nafasi ya kusikilizwa. Hatua hii inatupa moyo mkubwa kwa sababu tunatambua kuwa bado tuna umuhimu katika jamii na mchango wetu unatambuliwa. Tunaahidi kuendelea kuwa mfano mwema, kutumia hekima tuliyonayo kushauri na kuongoza vizazi vijavyo katika misingi ya maadili na uzalendo,” amesema Atanasi