WANANCHI IBUENI MIRADI YA MALEZI NA MAKUZI BORA YA WATOTO ILI KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI – WAZIRI DKT. GWAJIMA
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Makete, Njombe
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wananchi kuibua na kuwekeza katika miradi ya malezi na makuzi bora ya watoto kuanzia ngazi ya familia na jamii kwani hatua hiyo itasaidia kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na tabia nyingine hatarishi, huku ikijenga kizazi chenye maadili, uzalendo na uwajibikaji kitakachochangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 8 Julai, 2026, wakati akizindua Kituo cha Afya cha Kipagalo katika ziara yake ya kikazi wilayani Makete, mkoani Njombe, wakati .
"Tunapoibua na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kama barabara, maji, umeme na mingineyo, tusisahau pia kuibua miradi ya malezi na makuzi bora ya watoto. Huu nao ni uwekezaji muhimu kwa Taifa, kwa sababu malezi bora ndiyo suluhisho la kudumu la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na kujenga kizazi chenye fikra chanya," amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, Dkt. Gwajima amewataka wanafunzi wa kike na wa kiume kusoma kwa bidii, kujiepusha na watu wenye mienendo isiyo ya maadili, matumizi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni na vishawishi vinavyoweza kuharibu ndoto zao kwakuwa elimu ndiyo msingi wa mafanikio ya maisha, huku akiwahimiza kutunza miundombinu ya shule na kutumia fursa walizopewa kujenga maisha yao na kulitumikia Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Makete, Mhe. Kissa Gwakisa, amemshukuru Dkt. Gwajima kwa kufanya ziara ya kikazi wilayani humo, ambayo imekuwa chachu ya kuhamasisha wananchi na viongozi kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
" Maelekezo uliyoyatoa kuhusu malezi na makuzi bora ya watoto, pamoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi, yamepokelewa na yatafanyiwa kazi kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi zote ili kuendelea kuimarisha ustawi wa jamii wilayani Makete." amesema DC Kissa