WAKUU WA VYUO NA WARATIBU WA MADAWATI YA JINSIA WATAKIWA KUZINGATIA MWONGOZO ILI KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATILI VYUONI

Na WMJJWM - Tabora
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewataka Waratibu madawati ya Jinsia katika Vyuo Vikuu na vya Kati kuzingatia Mwongozo wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa madawati hayo ili kupambana na vitendo vya ukatili.
Wakili Mpanju ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya kuanzisha na kuendesha Madawati ya Jinsia katika vyuo vya elimu ya juu na kati kwa mikoa ya Tabora na Singida Juni 5, 2025.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Tabora, Wakili Mpanju, amesisitiza umuhimu wa madawati hayo katika kuwalinda wanafunzi, wahadhiri na jamii inayozunguka taasisi za elimu.
Wakili Mpanju amewataka wakuu wa vyuo kusimamia utekelezaji wa madawati hayo kwa ufanisi na kutoa wito kwao kuwa watekelezaji na watendaji katika kuhakikisha madawati haya yanaanzishwa na yanasimamiwa kwa kufuata mwongozo ili yalete matokeo chanya.
“Lengo la kuanzisha madawati haya ni kuzuia ukatili wa kijinsia na kuhakikisha huduma, ushauri nasaha na taarifa muhimu zinapatikana kwa wanafunzi, wakufunzi na jamii zinazozunguka vyuo.” amesema Wakili Mpanju
Wakili Mpanju amebainisha kuwa hadi sasa madawati ya jinsia 360 yameshaanzishwa nchini katika mikoa 11 na Serikali inalenga kufikia vyuo vyote 612 katika mikoa yote 26 nchini .
Akitoa salamu za Mkoa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Mhandisi Faustin Tarai, amesema kuwa mkoa huo umejipanga vyema kupambana na ukatili kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa mkoani humo katika kupambana na ukatili, zikiwemo kuanzishwa kwa madawati ya ulinzi wa mtoto mashuleni, utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari vya ndani na huduma jumuishi za msaada kwa wahanga wa ukatili kupitia hospitali ya rufaa ya Kitete.
Naye Mkurugeni Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia Rennie Gondwe amesema kuwa takriban wakuu wa vyuo 50 wamepatiwa Mafunzo ya Mwongozo kuhusu uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa Madawati ya Jinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na Kati, ambapo kati ya hao 21 ni kutoka mkoa wa Singida na 29 kutoka mkoa wa Tabora.
“Kupitia mafunzo haya, Wakuu wa Vyuo wataweza kusimamia kwa weledi uanzishwaji na uendeshaji wa madawati ya jinsia vyuoni, jambo ambalo litasaidia kuimarisha mifumo ya utoaji wa msaada kwa wahanga wa ukatili na kuhakikisha vyuo vinakuwa sehemu salama kwa wote,” amesisitiza Rennnie
Kwa niaba ya Wakuu wa Vyuo walioshiriki mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Tabora Polytechnic Juma Mudimi ametoa shukrani kwa Wizara kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu na kusema kuwa wamepokea kwa uzito mkubwa maelekezo yote yaliyotolewa na watahakikisha wanayatekeleza ipasavyo katika vyuo vyao.
“Tunaahidi kwenda kuyafanyia kazi mafunzo haya kwa vitendo, ili kuhakikisha taasisi zetu zinakuwa maeneo salama yenye usawa wa kijinsia na huru dhidi ya ukatili.” amesema Mudimi.