WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO WAIPA KONGOLE SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI NCHINI.

Na WMJJWM, Dodoma
Viongozi wa Makundi ya Wafanyabiashara ndogondogo wameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi za kuweka mazingira wezeshi kwa Wafanyabiashara ndogondogo hasa katika upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwao.
Hayo yamebainika wakati Viongozi hao walipokutana na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 6 Juni, 2025.
Mmoja wa Viongozi wa Makundi hayo Christian Msumali amesema mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kupitia Uratibu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI imewasaidia Makundi mbalimbali ya wafanyabiashara ndogondogo kupata fursa za mikopo ya kuendeleza na kukuza biashara zao.
Akizungumza na viongozi hao Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi na Wizara nyingine katika kuwafikia na kuwaboresha mazingira wafanyabiashara ndogondogo nchini.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu amelitazama kundi la wafanyabiashara ndogondogo kwa ukaribu zaidi na ametoa fedha nyingi kupitia Benki ya NMB ili zikopeshwe kwa makundi haya kwa riba na masharti nafuu" ameeleza Dkt Jingu.
Aidha amefafanua kuwa Wizara inalenga kuona kundi hili linafanya kwa ufanisi na ubora shughuli za uzalishaji mali kwa kuwa na mazingira rafiki, elimu na uwezeshwaji.
"Tutashirikiana na Taasisi nyingine za fedha, Wizara na wadau wengine ili kufikia malengo yetu, mfano nyie wafugaji tutashirikiana na Wizara ya Mifugo ili mpate ujuzi wa namna bora ya kufuga na katika sekta nyingine vivyohivyo" amefafanua Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Makundi Maalum Juma Samwel amesema Kitengo hicho kitaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ili waweze kuchangamkia fursa za mkopo nafuu wa asilimia saba iliyowekwa na Serikali kupitia Benki ya NMB
Aidha baada ya mazungumzo hayo Dkt. Jingu aligawa miongozo ya Uratibu na Usajili wa wafanyabiashara ndogondogo nchini kwa viongozi wa wafanyabiashara hao.
MWISHO