WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO SHINYANGA WAMEHAMASISHWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MIKOPO NAFUU YA SERIKALI

Na WMJJWM, Shinyanga
Wafanyabiashara ndogo katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo ya asilimia 7, inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Benki ya NMB.
Wito huo umetolewa Mei 14, 2025, na Maafisa wa Wizara kupitia operesheni maalum ya kutoa elimu kwa wajasiliamali ndogondogo kuhusu umuhimu wa kujisajili ili watambulike kama kundi maalum ambalo lipo katika mpango wa Serikali kuwakwamua kiuchumi kupitia mikopo yenye riba nafuu.
Akizungumza na wafanyabiashara hao Afisa Maendeleo kutoka Kitengo cha Makundi Maalum, Ezekiel Philipo amesema wafanyabiashara hao wanatakiwa kujisajili ili waweze kupata vitambulisho vitakavyowawezesha kufaidika na mikopo hiyo.
Amesema ili kupata mikopo hiyo ambayo ni lazima mfanyabiashara asajiliwe na kutambuliwa kwenye mifumo ndipo apate kitambulisho ambacho kitamsaidia kupata mikopo.
“Tumefika Shinyanga kutoa elimu kwa wafanyabiashara ndogondogo ili wachangamkie fursa ya kupata mikopo ya Serikali isiyo na dhamana, yenye riba nafuu ya asilimia 7 huku sharti pekee ni kuwa na kitambulisho kinachopatikana baada ya kusajiliwa rasmi,” amesema Philipo.
Aidha amesema mara baada ya kutoa elimu hiyo ya kujisajili na kutambuliwa, kwamba wanategemea kuona idadi kubwa ya wafanyabiashara hao katika Manispaa ya Shinyanga wanaongezeka kupata mikopo.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara hiyo David Malebetho amewataka wafanyabiashara hao kujitokeza kwa wingi kusajiliwa, akieleza kuwa hatua hiyo si tu itawasaidia kupata mikopo bali pia itawezesha Serikali kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara ndogondogo kwa ajili ya kupanga maendeleo kikamilifu.
Naye Mratibu wa zoezi la usajili na utambuzi wa wafanyabiashara ndogo Mkoa wa Shinyanga Rose Tungu, ambaye pia ni Afisa Biashara wa Mkoa huo, amesema bado kuna mwitikio mdogo wa kuchangamkia mikopo hiyo licha ya kuwa na masharti rafiki hivyo uhamasishaji huo utasaidia kuongeza mwamko kwa kwa wafanyabiashara.