Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA USALAMA WA MTOTO MTANDAONI

Imewekwa: 18 Jun, 2026
WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA USALAMA WA MTOTO MTANDAONI

Na Mwandishi Wetu, WMJJWM Dar Es Salaam.

Waandishi wa habari na waandaaji wa vipindi vya watoto nchini wametakiwa kutumia vyombo vyao vya habari kuelimisha jamii kuhusu usalama wa watoto mtandaoni ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili na matumizi mabaya ya teknolojia yanayowaathiri watoto.

Wito huo umetolewa na Afisa wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania, Prudence Constantine, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari na waandaaji wa vipindi vya watoto kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Prudence amesema maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yameleta manufaa makubwa katika upatikanaji wa taarifa, elimu, burudani na biashara, lakini pia yameongeza hatari mbalimbali zinazowakabili watoto wanapotumia mitandao bila uangalizi wa kutosha.

Amesema waandishi wa habari wana jukumu muhimu la kuelimisha wazazi, walezi na jamii kuhusu matumizi salama ya mtandao pamoja na madhara yanayoweza kuwapata watoto wanapotumia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.

Akizungumzia hali halisi, Prudence amesema utafiti uliofanyika mwaka 2022 kwa watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 ulibaini kuwa asilimia 67 ya watoto nchini wanatumia mtandao, huku mitandao maarufu ikijumuisha Facebook, Instagram, WhatsApp, TikTok na Telegram.

Amesema utafiti huo pia umeonesha kuwa baadhi ya watoto wamekumbana na aina mbalimbali za ukatili mtandaoni ikiwemo unyanyasaji, vitisho, ulaghai na kushawishiwa kutuma picha zisizofaa, hali inayohitaji hatua za haraka za kinga na elimu.

Kwa mujibu wa Prudence, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto kupitia marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Awali, Afisa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Octavian Peter, amesema matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto, jambo linalohitaji ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha watoto wanatumia teknolojia kwa usalama.

slot gacor