TUTIMIZE VEMA WAJIBU WETU KWA MATOKEO YENYE TIJA KWA MANUFAA YA JAMII - WAZIRI DKT. GWAJIMA
Na Said Said – Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa rai kwa watumishi wa wizara hiyo kuwekeza mioyo, nguvu na akili zao katika kuwatumikia wananchi kwa weledi na kujituma ili kupata matokeo yenye tija kwa manufaa ya jamii, ikiwemo wao wenyewe.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 16 Januari, 2026, wakati wa kikao cha mwanzo wa mwaka kati yake na watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara, Mji wa Serikali – Mtumba, mkoani Dodoma. Katika kikao hicho, Waziri aliwapongeza watumishi kwa kazi nzuri waliyotekeleza mwaka 2025 na kuwasisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia zana ya kufanyia kazi (instrument)
Amesema wizara inaanza mwaka 2026 ikiwa na mwelekeo na nyenzo rasmi ya utekelezaji wa majukumu, hivyo ni wajibu wa kila mtumishi kuielewa na kuitumia ipasavyo sambamba na kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 –2050 ili kuhakikisha maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanatekelezwa kikamilifu.
“Tunaanza mwaka huu tukiwa na (instrument) yetu ya wizara hii ya kufanyia kazi hivyo, natumaini watumishi wote wataweza kujengewa uwezo wa kuelewa majukumu yetu na vilevile, kukumbuka pia kuwa, tunatakiwa kutembea na dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 pamoja na miongozo mingine yote muhimu ili kuhakikisha maono ya Rais wa nchi yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanatekelezwa kikamilifu” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Mhandisi Maryprisca Mahundi amewasisitiza watumishi hao kuishi kwa upendo baina yao wenyewe lakini pia kuwahudumia wananchi kwa upendo wa dhati.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalum Dkt John Jingu amesema vikao hivyo baina ya viongozi na watumishi vina tija na umuhimu katika utumishi wa umma na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe.Waziri.