TAFITI SAHIHI NA UBUNIFU WA KIDIJITALI VITABORESHA UWEZESHAJI WA WATU NA USTAWI WA JAMII - WAZIRI DKT. GWAJIMA
Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dar es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema tafiti na ubunifu wa kidijitali vina mchango mkubwa katika kuboresha sera, mipango na huduma za ustawi wa jamii pamoja na uwezeshaji wa wananchi.
Dkt. Gwajima amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Uwezeshaji wa Watu na Ustawi wa Jamii lililofanyika tarehe 05, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kujadili masuala ya ujumuishaji wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, ulinzi wa watoto, afya ya akili, hifadhi ya jamii pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali na Akili Mnemba (AI) katika kuimarisha ustawi wa jamii. Aidha, amesisitiza kuwa maeneo hayo yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupata mafanikio katika maendeleo ya kijamii, ikiwemo kuboresha huduma za afya, kuimarisha ulinzi wa watoto na kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Gwajima amesema maarifa na mapendekezo yatakayotokana na kongamano hilo yatachangia maboresho ya sera na huduma katika maeneo muhimu kama ulinzi wa watoto, afya ya akili, hifadhi ya jamii, ujumuishaji wa watu wenye ulemavu na matumizi salama ya teknolojia za kidijitali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni, amesema kongamano hilo limewakutanisha washiriki zaidi ya 250 kutoka nchi 11 za ndani na nje ya Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujadili tafiti na kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya ustawi wa jamii. Amesema matarajio ya kongamano hilo ni kupata ushahidi utakaosaidia uwekaji wa sera, kuimarisha tafiti na kujenga mtandao mpana wa watafiti, wadau na watunga sera.