Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SIMAMIENI HUDUMA ZA USTAWI KWA VITENDO KULETA MAENDELEO : DKT. JINGU

Imewekwa: 02 Sep, 2025
SIMAMIENI HUDUMA ZA USTAWI KWA VITENDO KULETA MAENDELEO : DKT. JINGU

Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Wizara, Taasisi na Mashirika binafsi, zimetakiwa kutekeleza utoaji wa huduma za ustawi wa Jamii kwa vitendo ili kuwa na jamii yenye uwezo wa ustahimilivu na yenye mchango wa kuleta maendeleo kwa mtu, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa mkoani Dar Es Salaam Agosti 30, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango wakati wa Kilele cha Wiki ya Ustawi wa Jamii kilichofanyika katika Viwanja vya Ustawi wa Jamii Kijitonyama.

Dkt. Jingu amesema uhitaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini umeendelea kuongezeka kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kutokana na mabadiliko katika nyanja mbalimbali za maisha yakiwemo ya uchumi, siasa, jamii.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, wadau wa maendeleo na mashirika ya hiari inashughulikia changamoto zinazowakabili makundi maalum na jamii kwa ujumla.

"Natoa rai kwa wazazi/walezi na watanzania kwa ujumla kulinda haki na Ustawi wa Jamii kwa watoto wetu ili kuilinda nguvu kazi ya Taifa kwa maisha ya baadae. Kwani ulinzi na usalama wa watoto wetu ni jukumu letu sote." amesema Dkt. Jingu


Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la UNICEF Elke Wisch akitoa salamu zake wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na Wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma Bora kwa watoto kwenye Vituo vya Kulelea Watoto mchana, Makao ya Watoto na Nyumba Salama zinatolewa kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Children in Crossfire (CIC) Craig Fera akitoa salamu zake wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo amesema huduma za ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika jamii hasa katika hatua za mwanzo za binadamu za ukuaji wa watoto hivyo sekta ya Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana ni Msingi katika Ustawi na Maendeleo ya Jamii