SERIKALI YAWAKARIBISHA WADAU KUTOA HUDUMA ZA MALEZI NCHINI.
YALITAMBUA SHIRIKA LA COMPASSION INTERNATIONAL TANZANIA KAMA MFANO WA KUIGWA.
Na Maryam Elhaj WMJJWM- Arusha
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imewakaribisha wadau mbalimbali kuwekeza katika vituo Malezi kwa watoto ili kuunga mkono juhudi zake katika kuhakikisha watoto wanapata malezi stahiki.
Hayo yamebainika Mkoani Arusha tarehe 6 Desemba 2025, wakati wa ziara kujionea huduma zinazotolewa na Vituo vya malezi vinavyosimamiwa na Shirika la Compassion International Tanzania, Wilayani Monduli ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuimarisha ustawi na ulinzi wa mtoto nchini.
akizungumza wakati wa ziara hiyo Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Faithmary Lukindo amesema Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2024/25–2028/29, ukiwa na lengo la kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2029.
“Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya malezi kwa kushirikiana na Wizara za kisekta, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wa maendeleo na kusizitiza kuwa kazi inayofanywa na Shirika hili imekuwa chachu katika kuboresha ustawi wa mtoto kwa kutoa huduma muhimu kama lishe, elimu, malezi ya awali, ulinzi na mafunzo ya stadi za maisha”amesema Faithmary.
Aidha Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku, ameeleza kwamba lengo la ziara hiyo ni mwendelezo wa kikao cha robo mwaka cha Kikundi Kazi cha Malezi Taifa kilichofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 03–05 Desemba 2025 na kufanya thathimini ya utekelezaji wa majukumu ya Kikundi Kazi hicho.