SERIKALI YASISITIZA UWEKEZAJI KWA VIJANA BALEHE KUIMARISHA AFYA, ELIMU NA USTAWI WA TAIFA
Na, Oscar Tarimo, WMJJWM – DODOMA
Serikali inaendelea kuimarisha uwekezaji kwa vijana balehe kama msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, Ili kuhakikisha kundi hilo linapata fursa bora za afya, elimu na ustawi.
Hayo yamesemwa leo Aprili 23, 2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, wakati akifungua mkutano wa wadau wa kupokea matokeo ya tathmini Utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe ( NAIA).
Amesema vijana ni nguzo muhimu ya maendeleo ya sasa na baadaye, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa hatua madhubuti zinazolenga kulinda afya, elimu na ustawi wao ili kuhakikisha wanakuwa na mchango chanya katika maendeleo ya taifa
.“Uwekezaji katika afya na elimu ya vijana balehe ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye maendeleo endelevu na rasilimali watu imara,” amesema Mpanju.
Akieleza mafanikio ya utekelezaji wa ajenda hiyo iliyoanza mwaka 2021, Mpanju amesema kumekuwa na matokeo chanya katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kupungua kwa maambukizi ya VVU, mimba za utotoni na ukatili dhidi ya watoto. Aidha, amesema juhudi za kuboresha lishe na upatikanaji wa elimu zimeendelea kuonesha mafanikio ya kuridhisha katika baadhi ya mikoa ya nchi.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa kwa umakini, akibainisha kuwa matokeo ya tathmini hiyo yatasaidia kubaini mapungufu na kuweka mikakati mipya yenye tija zaidi kwa awamu ijayo ya utekelezaji.
Mpanju pia amesisitiza kuwa mkutano huo unatoa fursa muhimu kwa wadau wa maendeleo kuchambua mafanikio na changamoto, na kuandaa dira bora ya uwekezaji kwa vijana balehe.
Aidha, amewashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa mchango wao katika utekelezaji wa ajenda hiyo, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja kati ya Serikali na wadau hao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mtoto, sehemu ya Maadili na Maendeleo ya Mtoto, Asha Shame, amesema upokeaji wa matokeo hayo ni sehemu ya kujipima mafanikio dhidi ya malengo na mikakati iliyowekwa.
"Tathmini hii imejikita katika maeneo matano ikiwemo upimaji wa matokeo, uratibu wa uwajibikaji katika ngazi ya taifa, ushiriki wa vijana, mafunzo pamoja na kubainisha changamoto na mafanikio, sambamba na kutoa mapendekezo ya hatua zijazo" amesema Asha.
Naye Dkt. Ahmad Mukuwani, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, amesema Ajenda ya Taifa ya Kuwekeza katika Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe (NAIA) imekuwa na mchango mkubwa katika kuwahamasisha vijana kujiunga na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA), hatua inayowawezesha kupata ujuzi wa kujitegemea na kuchangia ukuaji wa uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.