Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SERIKALI YASHIRIKI KIKAO CHA NGAZI YA JUU KUHARAKISHA JUHUDI ZA KUTOKOMEZA NDOA ZA UTOTONI AFRIKA

Imewekwa: 17 Feb, 2026
SERIKALI YASHIRIKI KIKAO CHA NGAZI YA JUU KUHARAKISHA JUHUDI ZA KUTOKOMEZA NDOA ZA UTOTONI AFRIKA

Na Mwandishi wetu, Addis Ababa, Ethiopia

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeshiriki katika kikao cha pembeni cha ngazi ya juu kilichofanyika sambamba na Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika, kikilenga uzinduzi wa Ripoti ya Bingwa wa mwaka 2025 kuhusu kutokomeza ndoa za utotoni pamoja na Mpango wa Spotlight – Programu ya Kikanda ya Afrika 2.0. Mpango huo unalenga kuharakisha juhudi za kulinda haki za mtoto wa kike na kuwawezesha wanawake na wasichana barani Afrika.

Katika kikao hicho, Serikali iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi. Kikao hicho kiliongozwa na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ambaye ni Bingwa wa Umoja wa Afrika katika kampeni ya kutokomeza ndoa za utotoni barani Afrika.

Majadiliano yaliwakutanisha viongozi wa serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo, yakijikita katika tathmini ya mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazoendelea pamoja na hatua zinazotekelezwa na nchi wanachama kupunguza na hatimaye kumaliza ndoa za utotoni. Washiriki pia walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mikakati ya pamoja ya kikanda, kisera na kifedha ili kuongeza kasi ya juhudi hizo pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Aidha, kikao hicho kilisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Afrika Tunayoitaka, inayolenga kujenga bara lenye usawa, ustawi na heshima kwa haki za wanawake na watoto.