SERIKALI NA WADAU WA MAENDELEO WAJIDHATITI KUIMARISHA MALEZI.
Na WMJJWM- Arusha
Serikali imesema inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo elimu kwa jamii kuhusu malezi na familia.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha robo mwaka cha Kikundi Kazi cha Malezi Taifa kilichofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 03-05 Desemba, 2025.
Akizungumza wakati wa Kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku amesema katika kuboresha uratibu wa afua za malezi, Wizara imeanzisha Kikundi Kazi cha Malezi Taifa, kwa lengo la kupitia na kujadili utekelezaji wa afua mbalimbali za malezi na matunzo ya watoto nchini.
Ameongeza kuwa kupitia Kikundi hicho cha Kitaifa cha Malezi kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo inaendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) 2024/25–2028/29, wenye lengo la kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2029.
“Kwa robo ya pili ya mwaka huu, kikundi kazi hiki kinachoundwa na Wizara za kisekta, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN Agencies) kimekutana jijini hapa kujadiliana masuala mbalimbali yahusuyo Malezi “ amesema Kitiku.
Ameongeza kuwa Wizara inahimiza ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha juhudi za kuimarisha malezi, ustawi na ulinzi wa mtoto ili kufikia Tanzania isiyo na ukatili kwa wanawake na watoto.
Nao baadhi ya Wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Mashirika ya Kimataifa wamesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kutoka Wizara na Taasisi za Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na Jamii inaondoka na Vitengo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Mkutano huo umejikita katika kupokea na kujadili mawasilisho ya wadau wanaotekeleza afua za malezi nchini, kubadilishana uzoefu na kuimarisha mifumo ya uratibu na kupanga maboresho ya utekelezaji wa mpango kazi wa malezi katika ngazi zote.