Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SERIKALI KUWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA BIASHARA NDOGONDOGO, IKIWEMO KUNDI LA MAMA LISHE

Imewekwa: 22 Apr, 2026
SERIKALI KUWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA BIASHARA NDOGONDOGO, IKIWEMO KUNDI LA MAMA LISHE

Na WMJJWM - Dar Es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha biashara ndogondogo ikiwemo kundi la mama na baba lishe kwa kuzingatia Dira ya maendeleo ya taifa ya 2050 inayolenga kukuza uchumi jumuishi na unaowanufaisha wananchi wote.

Rais samia ameyasema hayo leo tarehe 21 April, 2026 katika kongamano la kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania lililofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa serikali inatambua nafasi ya sekta isiyo rasmi katika kufunikisha malengo ya Dira ya Taifa , hususani katika kupunguza umasikini ,kuongeza ajira na kuinua kipato cha wananchi.

Ameongeza kuwa Ilani ya CCM inaelekeza kuwepo kwa mazingira bora ya uwezeshaji kiuchumi kwa makundi yote, wakiwemo mama na baba lishe ambao ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani katika huduma ya chakula, na hilo ndilo kusudi la uwepo wa Kongamano hilo kutimiza ahadi walizotoa na mikakati ya kuinua wananchi kiuchumi kama ambavyo Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyosema.

" Tunataka kuona mama na baba lishe wakikua kutoka biashara ndogondogo kwenda za kati na hatimaye kuwa wajasiliamali wakubwa, tutahakikisha tunawatengenezea mazingira wezeshi kwa kuwapa mikopo yenye masharti nafuu na kuwatengenezea miundombinu wezeshi katika shughuli zenu ikiwemo matumizi ya nishati safi,” ameeleza Rais Samia.

Aidha, amesema kuwa ili kukamilisha lengo la kuwainua na kuwaimarisha mama na baba lishe Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa mikopo kupitia halmashauri, kutoa mafunzo ya ujasiliamali pamoja na kuhakikisha kuwepo kwa maeneo rasmi na salama ya kufanyia biashara zao ,hatua ambazo zinakwenda sambamba na utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Taifa.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara imeendelea kushirikiana na Kundi la Mama na Baba Lishe Tanzania kwani ni Kundi ambalo linachangia Uchumi wa nchi kwa kutoa ajira na huduma ya chakula kwa jamii.