SERIKALI KUBORESHA MWONGOZO WA UTEKELEZAJI WA MASUALA YA JINSIA.
Na, Oscar Tarimo, WMJJWMM-Morogoro
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, ametoa wito umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau katika kuimarisha utekelezaji wa ajenda ya usawa wa kijinsia nchini.
Felister amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha kupokea maoni ya wadau kutoka Taasisi za umma na zisizo za Kiserikali, Wizara mbalimbali nchini na wadau wa masuala ya kijinsia kwa ajili ya kuboresha Mwongozo wa Uzingatiaji, Uratibu na Utekelezaji wa Masuala ya Jinsia, Machi 26, 2026 mkoani Morogoro.
Amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sera, sheria na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha masuala ya jinsia yanapewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya Taifa.
Ameeleza kuwa mwongozo huo utasaidia kuweka mfumo madhubuti wa uratibu na ufuatiliaji wa utekelezaji wa masuala ya jinsia katika sekta zote, jambo litakalosaidia kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wake.
“Tunatarajia kupitia kikao hiki tutapata maoni yenye tija yatakayosaidia kuboresha mwongozo huu ili uweze kutekelezeka kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika jamii.” amesema Mdemu.
Sambamba na hilo, amewasihi washiriki kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi za umma, sekta binafsi na asasi za kiraia kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha usawa wa kijinsia, akibainisha kuwa ushirikiano wa wadau ni msingi muhimu wa kufanikisha maendeleo jumuishi nchini.
Kwa upande wake, Mshauri Mwandamizi wa Uratibu wa Masuala ya Kijinsia na Wanawake, Amani na Usalama kutoka UN Women, Usu Mallya, amesema watahakikisha uzingatiaji wa masuala ya kijinsia unatekelezwa ipasavyo sambamba na kufanya tathmini ya hali ya usawa wa kijinsia.
Kikao hicho kimeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana Ubalozi wa Ireland na Shirika la UN Women.