Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

‎SERIKALI INAJALI MASLAHI YA WAFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO - DKT. MWIGULU NCHEMBA

Imewekwa: 17 Jan, 2026
‎SERIKALI INAJALI MASLAHI YA WAFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO - DKT. MWIGULU NCHEMBA

‎Serikali yajidhatiti kuhakikisha wafanyabiashara ndogondogo wanainuka kiuchumi kwa kuweka mazingira wezeshi na mipango madhubuti  inayoimarisha uratibu na usimamizi wao nchi nzima.

‎Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba alipokuwa akizungumza  katika Kongamano la Wamachinga, madereva pikipiki bajaji za kubeba abiria, Mama Lishe na Baba Lishe   Januari 08, 2025 Jijini Dar Es Salaam.

‎Dkt Mwigulu amesema Serikali sikivu chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imesikia na kuzingatia hoja za wafanyabiashara ndogondogo  wanazokumbana nazo na kuahidi kukaa na Wizara zinazohusika na Makundi hayo na kuweka mikakati ya kutatua changamoto hizo.

‎“Tutakaa pamoja na Mawaziri wa Wizara zinazowaratibu hivyo nawaomba mtoe fursa kwa Serikali kwa kushirikiana na viongozi wenu kutafakari ili tufanye jambo ambalo litawarahisishia shughuli zenu” amesema Dkt. Mwigulu.

‎Vilevile Dkt. Mwigulu amesema  kwamba katika miaka mitano ijayo kuanzia mwaka wa fedha wa 2025/2026 Serikali itaongeza fedha ya mafungu ya vijana,wanawake na Makundi Maalum kwa ajili ya makundi hayo.

‎Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Dkt  Dorothy Gwajima amebainisha juhudi zilizokwisha  chukuliwa na Wizara kwa kushirikiana na Wizara nyingine katika kuwainua wafanyabiashara ndogondogo toka ilipokabidhiwa jukumu ya kuwaratibu na kuwasimamia wafanyabiashara ndogondogo.

‎“Tulianza na programu ya kuwatambua wafanyabiashara ndogondogo kupitia mfumo wa kidigitali ambapo waliotambuliwa ni 115794 na katika kuimarisha elimu hii yamefanyika makongamano mikoa yote kasoro mmoja tu na Mikoa  21 imeshajenga Ofisi za Machinga kasoro miaka 5 ya Simiyu, Mwanza, Singida,Kigoma, Rukwa bado inaendelea na ujenzi” amesema Dkt. Gwajima

‎Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara ndogondogo SHIUMA Ernest Matondo ameishukuru Serikali kwa jitihida za kuwasikiliza na kuhakikisha  wanainuka na kuwa na mazingira rafiki ya kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwatengea maeneo na kuwajengea ofisi za machinga nchi nzima