Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SERIKALI IMEJIPANGA KUIMARISHA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025 – WAZIRI GWAJIMA

Imewekwa: 17 Jun, 2025
SERIKALI IMEJIPANGA KUIMARISHA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UCHAGUZI MKUU 2025 – WAZIRI GWAJIMA

Na WMJJWM – Dar Es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara yake imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha ushiriki wa wanawake katika siasa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unazidi kuimarika.

Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo katika kikao maalum cha Tathmini ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Umoja wa Afrika, uliofanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 16 Juni 2025, na kuhudhuliwa na viongozi waandamizi kutoka Umoja wa Afrika, akiwemo Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka na Jaji Effie Owuor.

Amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wanawake kupitia marekebisho ya sheria na sera mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa lengo la kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi ya kisiasa. Ametaja mafanikio yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na ongezeko la uwakilishi wa wanawake bungeni kutoka asilimia 21 mwaka 1995 hadi kufikia asilimia 37 kwa sasa. Vilevile, ameeleza kuwa nafasi za wanawake katika ngazi za Ukuu wa Mikoa na Wilaya zimeongezeka kwa kiwango kikubwa, jambo linaloonesha dhamira ya kweli ya Serikali katika kufanikisha usawa wa kijinsia.

Aidha, Dkt. Gwajima ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kujenga mazingira ya kisiasa jumuishi, hasa kwa kuwezesha wanawake kushiriki kwenye siasa kupitia mfumo wa uwakilishi wa asilimia 30 pamoja na utekelezaji wa programu kama Wanawake Wanaweza, inayolenga kujenga uwezo wa uongozi kwa wanawake na vijana wa kike.

Hata hivyo, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Wizara imejipanga kuongeza juhudi zaidi katika kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kuhakikisha vyama vya siasa vinafuata kikamilifu Sera ya Kijinsia, iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Tanzania inathibitisha tena dhamira yake ya kulinda haki za wanawake na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa mwaka 2025, huku ikizingatia usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa makundi yote katika jamii,” amesema Dkt. Gwajima.