Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

NAIBU WAZIRI MWANAIDI KUZINDUA KITINI CHA UWEZESHAJI  MAJADILIANO YA MILA NA DESTURI NGAZI YA JAMII IKUNGI SINGIDA.

Imewekwa: 02 Jun, 2025
NAIBU WAZIRI MWANAIDI KUZINDUA KITINI CHA UWEZESHAJI  MAJADILIANO YA MILA NA DESTURI NGAZI YA JAMII IKUNGI SINGIDA.

Na WMJJWM, Ikungi Singida.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, anatarajiwa kuzindua kitini cha wawezeshaji kuhusu majadiliano ya mila na desturi ngazi ya Jamii ikiwa ni Kampeni ya Mageuzi ya Kifikra na mitazamo ya Jamii kuwa kitovu cha maendeleo Juni 2, 2025 katika Wilaya ya Ikungi.

Hayo yamebainika wakati timu ya Wataalam lkutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kufanya majadiliano na wanakijiji wa Makhonda Wilayani Ikungi Mkoani Singida Mei 30, 2025.

Akizungumza na wanakijiji hao kiongozi wa msafara huo Zukra Mangachi ameeleza kuwa wamefika kijijini hapo kwa lengo la kuendesha  majadiliano ya Mila na desturi ngazi ya jamii na kuhusu kampeni ya amsha ari yenye mlengo wa  kugeuza fikra za wananchi kuwa kitovu cha maendeleo ngazi ya jamii pamoja na maandalizi ya uzinduzi wa kitini cha uwezeshaji wa majadiliano ya mila na desturi katika jamii.

"Tumekuja tujadiliane pamoja kuhusu mila zetu zipi zinafaa kuendelea kufuatwa na zipi hazifai, pia tujadili kuhusu maendeleo kwa kuwa tunaposema nyinyi ni kitovu cha maendeleo tunamaanisha kuwa mnahitaji kupanga, kutekeleza na hata kuitunza miradi yenu" ameeleza Zukra.

Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makhonda Rungwando Kashinje amewashukuru timu ya Wataalam hao kwa kuwafikia na kuwapatia elimu yenye manufaa kwao.

"Sisi wanakijiji wa Makhonda tumepokea kwa heshima kubwa elimu hii kwa kuwa mengi mmetufundisha ni ya msingi kwenye jamii yetu" ameeleza Mwenyekiti Kashinje.