MSAJILI WA NGOs,NACONGO WAIMARISHA USHIRIKIANO
Na Augustina Makoye WMJJWM- Dodoma
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs imeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) katika kuhakikisha usimamizi na uratibu wa shughuli za Mashirika hayo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa, ili kuzuia muingiliano wa kazi na kuimarisha ushirikiano kati ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Serikali.
Hayo yamebainika katika kikao cha pamoja kati ya Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na NACONGO kilichofanyika Machi 26, 2026, katika Ukumbi wa Wizara, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadili mafanikio ya utekelezaji wa malengo ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha, kuanzia Januari hadi Machi, 2026 pamoja na mchakato wa marekebisho ya kanuni na miongozo ya uendeshaji wa Baraza hilo.
Aidha, walijadili mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa maazimio ya kikao cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo kamati za kuendesha majukwaa ziliundwa. Vilevile, mchakato wa maboresho ya muundo na kanuni za uendeshaji wa Baraza unaendelea ili kuongeza ufanisi, pamoja na kuweka uwakilishi kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.
Katika hatua nyingine, Wizara kwa kushirikiana na NACONGO ilifanikiwa kuratibu ushiriki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2025 kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi tofauti kuanzia msingi hadi kitaifa.
Ushirikiano huo umewezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupata mwongozo wa kisera kutoka serikalini, hatua iliyosaidia kuyawezesha kuelewa sera za kitaifa na kuziunganisha na shughuli zao za kila siku. Hali hii imepunguza migongano ya kimkakati na kuongeza ufanisi wa miradi ya kijamii.
Kwa upande mwingine, Wizara imenufaika kwa kupata taarifa zikiwemo changamoto mashirika yaliyosajiliwa nchini na kushirikiana na NACONGO katika kuzitafutia ufumbuzi. Taarifa hizo zimekuwa muhimu katika kupanga sera zinazojibu mahitaji ya jamii.