Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MPANJU AAMSHA ARI KATA YA KIHONDA

Imewekwa: 01 Apr, 2026
MPANJU AAMSHA ARI KATA YA KIHONDA

Aongoza harambee  kuchangia ujenzi Kituo cha Polisi, atoa mifuko 45 ya saruji

Na WMJJWM - Morogoro

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amesema wananchi wanao wajibu wa kujiletea maendeleo kwa kushiriki, kujitolea  na kuchangia ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika maeneo yao. 
 
Mpanju amesema hayo Machi 31, 2026, baada ya kushiriki ujenzi wa kituo cha polisi kata ya Kihonda, Mtaa wa Kiagae A mkoani Morogoro.

Mpanju amesema ni muhimu wananchi kuwa na mtazamo chanya katika uchangiaji wa miradi ya kimaendeleo katika maeneo yao kwa sababu ndiyo wanaufaika wakuu wa miradi hiyo. 

"Naomba niwaase endeleeni kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu kwa sababu kwa njia hiyo tutaharakisha maendelo katika maeneo yetu, ujenzi wa kituo hiki cha polisi katika Kata ya Kihonda ni kwa ajili ya usalama wenu, jambo ambalo litawafanya ninyi kufanya shughuli za kimaendeleo kwa amani na utulivu”. amesema Mpanju. 

Pamoja na kushiriki shughuli hiyo ya kuamsha ari kwa jamii kwa ngazi ya msingi, ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha polisi ambapo amechangia mifuko 45 ya saruji pamoja na kuwachangisha wananchi zaidi ya Milioni sita papo kwa hapo. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Kihonda Tatu Ally ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuhamasisha wananchi kushiriki miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao, kwani njia hiyo inawafanya wananchi kuthamini miradi na kutunza miundombinu hiyo kwa maslahi yao. 

Aidha, Tatu amesema wananchi wa Kata hiyo wamekuwa mstari wa mbele katika ushiriki wa shughuli za maendeleo, kwani wameweza kujenga Ofisi ya Kata jambo ambalo linaendelea kutoa hamasa kwa wananchi katika ushiriki wa ujenzi wa miundombu ya maendeleo yao. 

MWISHO.