WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA “INSPIRE TO LEAD” ASISITIZA USHIRIKIANO KWENYE KUJENGA JAMII YENYE USAWA
WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA “INSPIRE TO LEAD” ASISITIZA USHIRIKIANO KWENYE KUJENGA JAMII YENYE USAWA
Na WMJJWM - DODOMA
Katika tukio la kihistoria lililofanyika Juni 25, 205 jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua kampeni ya Inspire to Lead yenye lengo la kuinua ushiriki wa wanawake na wasichana katika uongozi na sekta za kisayansi. Kampeni hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.
Akitoa hotuba yake Dkt. Gwajima amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuimarisha usawa wa kijinsia nchini na kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Alieleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha mafanikio makubwa katika juhudi hizi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza kasi hiyo kwa kushirikiana wadau wote.
Kampeni ya Inspire to Lead inalenga kubadili mitazamo ya kijamii kuhusu nafasi ya mwanamke, kukuza hali ya kujiamini kwa wanawake kushiriki uongozi, na kuwahamasisha wasichana kujiunga na masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM). Mbinu zitakazotumika ni pamoja na uandaaji wa video fupi za viongozi wanawake, pamoja na ujumbe wa kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari.
Dkt. Gwajima ametoa wito kwa wadau wote kuungana kwa nguvu kuhakikisha kuwa ujumbe wa kampeni unafika kila kona ya jamii ili kuleta mabadiliko ya kweli. “Kwa pamoja, tutaijenga jamii yenye usawa, haki na wanawake jasiri wanaoongoza katika kila nyanja,” alihitimisha.
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalum Wakili Amon Mpanju amefafanua kwamba Maendeleo yeyote ndani ya Jamii yanahitaji ushiriki wa kila mmoja pasipo kubagua jinsia.
“Kwa wajibu wa sensa ya 2022 takwimu zinaonyesha kuwa wanawake ni asilimia 51 ya wananchi na endapo wanawake wataweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji kiuchumi tutaweza kufikia uhuru wa kiuchumi kwa kila mtu”amesema Mpanju.