MIKOPO YA SERIKALI INAWASUBIRI: MPANJU
Na WMJJWM - MOROGORO
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Mpanju amewataka wananchi kuchangamkia mikopo yenye mashatri nafuu inayotolewa na Serikali ili waweze kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Mpanju amesema hayo Machi 31, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kihonda na Mkundi katika mkutano maalum wa kuhamasisha wananchi kuzitambua fursa mbalimbali za mikopo inayotolewa na serikali na taasisi zake kwa ajili ya kuinua wananchi kiuchumi.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Hassan Suluhu, imetoa fursa za mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili yenu, naomba mzichangamkie, kwa sababu hizo ni fedha ni kwa ajili yenu” amesema Mpanju.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, inaratibu mikopo kwa wafanyabiashara ndogondogo ambayo hutolewa na Benki ya NMB katika matawi yake yote nchini, hivyo kinachotakiwa ni wananchi kufuata taratibu za kukopeshwa fedha hizo kwa kufika katika ofisi za hamashauri zao.
Aidha amehamasisha vijana kuchangamkia mikopo inayotolewa na Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana ili waweze kunufaika na mikopo hiyo na kuleta maendeleo katika jamii na Taifa.
Akitoa uhsuhuda namna alivyonufaika na mkopo wa asilimia kumi unaotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Omari Delalile amesema mkopo huo umewasadia kukuza biashara yao ya karakana ya useremala na hivyo wameweza kuongeza faida pamoja na kurejesha bila changamoto.
“Kikundi chetu tupo jumla ya watu watano, tulikopeshwa jumla ya shilingi milioni thelasini na tano (35,000,000), tunawashukuru maafisa maendeleo ya jamii, maafisa biashara pamoja na uongozi wote wa Halmashauri ya Morogoro kwa kutusimamia, kutupa mafunzo ya uendeshaji wa biashara yetu baada ya kupata mkopo huu”
Omari ametoa wito kwa vijana kuthubutu na kuchukua mikopo inayotolewa na serikali kwa sababu haina mashatri magumu badala ya kujiingiza katika mikopo ya kausha damu ambayo ina masharti magumu.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB tawi la Morogoro mjini Lilian Abraham amewahamasisha wananchi kuendelea kuchukua mikopo inayotolewa na Serikali akisema hadi sasa ni watu zaidi ya 150 ndio walichukua mkopo huo katika Halmashauri ya Morogoro, huku akisema fedha bado zipo za kutosha na kutoa wito kwa wananchi kufika katika matawi ya NMB kuchukua mikopo hiyo.
MWISHO