Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

KAMATI YA MTAKUWWA KATA YA CHAMWINO MOROGORO YAPONGEZWA

Imewekwa: 25 Mar, 2026
KAMATI YA MTAKUWWA KATA YA CHAMWINO MOROGORO YAPONGEZWA

Na WMJJWM, Morogoro

Kamati ya Mpango wa Taifa wa Kuzuia Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kata ya Chamwino mkoani Morogoro, imepongezwa kwa juhudi zake za kutoa huduma shirikishi hususani katika kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto.

Pongezi hizo zimetolewa Afisa Ustawi wa Jamii wa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum David Ntezidyo wakati wa ziara ya kisekta yenye lengo la kukagua uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili pamoja na kubaini mbinu mbalimbali za kupinga Ukatili katika Jamii.

Ziara hiyo iliyofanyika Machi 24, 2026 imehusisha Kituo cha Huduma kwa manusura wa Vitendo vya Ukatili cha Sabasaba na kutembelea kamati ya MTAKUWWA katika kata ya Chamwino.

Akiwasilisha taarifa ya kituo hicho, Afisa Ustawi wa Jamii Jamila Malinza, amesema uelewa umeongezeka kwa wananchi, jambo linalowasaidia kuripoti vitendo vya ukatili kwa wakati na kuwezesha mamlaka kuchukua hatua stahiki.

"Matukio ya ukatili yamepungua kutoka kesi 230 mwaka 2024 hadi kesi 208 mwaka 2026, hatua inayochangiwa na kuongezeka kwa elimu ya kuzuia ukatili kwa wananchi inayotolewa na Maafisa Ustawi wa Jamii ngazi ya kata kwa kushirikishana na Kamati za MTAKUWWA.

Aidha, Mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Banza amesema uwepo wa MTAKUWWA umechangia kupungua kwa vitendo vya ukatili kupitia utoaji wa elimu katika mitaa, nyumba kwa nyumba, shuleni na kwenye vikundi vya wanawake.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Amisa Kagomba, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto, ikiwemo kupitia majukwaa ya mtandao, pamoja na kuimarisha uwajibikaji wa kamati za MTAKUWWA ili kudumisha mafanikio hayo.

Ziara hiyo imehusisha pia wawakilishi kutoka Ofisi ya mwendesha mashtaka Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya katiba na Sheria

MWISHO.