KAMATI YA BUNGE YAPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII 2026/27
Na WMJJWM-Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha 2026/2027, baada ya kujadili na kuridhishwa na mwelekeo wa mpango na bajeti hiyo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Mchafu, amesema Kamati imejiridhisha na maandalizi ya bajeti hiyo pamoja na vipaumbele vilivyowekwa, hivyo kuidhinisha utekelezaji wake kwa lengo la kuendelea kuimarisha ustawi wa jamii nchini.
"Niwapongeza Wizara kwa maandalizi ya bajeti yenye mwelekeo wa kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja, mhakikishe fedha zilizoidhinishwa zinatumika kwa ufanisi na uwajibikaji." amesema Mhe. Hawa
Aidha Mhe. Hawa ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara katika kufuatilia utekelezaji wa bajeti hiyo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kwa wakati na kwa tija kwa jamii.
Awali akiwasilisha muhtasari wa randama ya mpango na bajeti hiyo, Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Wizara inaomba jumla ya Shilingi 83,524,243,000 kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Ameeleza kuwa fedha hizo zitatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha huduma za ustawi wa jamii, kukuza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha malezi na makuzi ya watoto.