DKT. JOHN JINGU AKAGUA HUDUMA NA MAENDELEO YA MAHABUSU YA WATOTO DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, Desemba 10, 2025 ametembelea na kukagua huduma na maendeleo ya Mahabusu ya Watoto Upanga Dar Es Salaam na kujionea utendaji kazi wa mahabusu hiyo.
Dkt. John Jingu amesisitiza kwamba Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda na kuwathamini watoto wote hata wale waliokinzana na sheria kwa kuhakikisha wanapata malezi na maisha bora wakiwa mahabusu.
Ameongeza kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa Watoto wanapotoka mahabusu wanakuwa na elimu na ujuzi wa kujitegemea katika kuendesha maisha yao.
Dkt. Jingu amewaasa watoto hao kuendelea kuwa watu wema na kuwasisitiza kuwa Serikali ipo pamoja nao na itaendelea kuwapatia huduma bora wakiwa katika mahabusu hiyo.
Aidha, Dkt. Jingu amewapongeza watumishi wa mahabusu hiyo kwa huduma wanayotoa kwa watoto waliopo hapo kwa moyo na upendo huku akipata wasaa wa kusikiliza kero zao, ambapo baadhi ya changamoto zilitolewa majibu papo hapo na nyingine akaahidi kufanyiwa kazi.
Akiwasilisha taarifa ya Mahabusu ya Watoto Upanga Dar Es Salaam, Afisa Mfawidhi wa Mahabusu hiyo, Joseph Charles Mwita, amesema Mahabusu hiyo ina watoto watano, mmoja wa kike na wanne wa kiume huku watoto hao wakifundishwa mambo mbali mbali ya kuongeza ujuzi.
"Watoto wanaoishi katika mahabusu hii wanajifunza dini, mambo ya kiraia, kilimo cha umwagiliaji, ufundi wa kunyoa nywele, ushonaji na utengenezaji wa shanga za urembo.” ameeleza Mwita.
Kwa upande wao watoto waliopo katika Mahabusu hiyo wamehaidi kuwa watoto wema katika jamii na mabalozi wazuri kwa watoto wengine na kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuajiri watu wengine.
MWISHO