DKT. BITEKO ASHAURI JAMÌI KUZINGATIA MALEZI BORA YA AWALI KWA WATOTO.

Na WMJJWM- Mwanza
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameitaka jamii kuzingatia malezi bora kwa watoto kuanzia ngazi ya familia ili waweze kukua katika maadili mema na kulitumikia taifa kwa uzalendo.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifunga Kongamano la Malezi katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia lililofanyika Mei 24, 2025 Jijini Mwanza.
Ameongeza kwamba familia inapaswa kumrithisha mtoto maadili na mila zinazofaa, hivyo kila mzazi anatakiwa kuchukua nafasi yake kuhakikisha mtoto analelewa ndani ya familia ili kuepuka watoto kuingia mitaani ambapo ni mazingira hatarishi kwa ustawi wao.
"Familia inajumuisha baba, mama na watoto na wote tunajua kwamba mtoto ni zao la upendo kati ya baba na mama hivyo ni muhimu mtoto akalelewa vizuri na hiyo ndiyo njia ya kuwa na taifa lenye watu wazalendo" amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika suala la malezi kwa familia hasa kutenga muda wa kuwa na familia na watoto kwani inasaidia kujenga upendo na maelewano katika familia.
"Mhe. Rais Samia alisema katika moja ya hotuba zake kuwa ukikosa muda wa kuwa na familia yako na watoto wako unajitengenezea upweke katika uzee wako, kwahiyo tuwe na muda na familia zetu hasa watoto wetu" amesisitiza Dkt. Biteko
Akitoa salamu katika kongamano hilo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwananidi Ali Khamis amesema Serikali inaendelea kutekeleza Programu mbalimbali za malezi ikiwemo kujenga vituo vya kulea watoto katika maeneo yenye shughuli za kijamii kama vile sokoni ili kuwezesha wazazi kuwapa watoto malezi bora, kuwajengea uwezo walimu wa awali kwa kutoa elimu ya watoto na kujenga vituo vya kulea watoto wadogo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda akitoa salamu katika kongamano hilo amewaasa watumishi wa umma kutojisahau katika malezi na makuzi ya watoto kutokana na majukumu yao mbalimbali ya utumishi serikalini.
Ameongeza kwamba ni muhimu jamii kuzingatia maadili ya kidini na kuepuka kuzaa nje ya ndoa ili kupunguza migogoro na matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa